Shirika la Habari la Hawza - Kwa kuwa lengo la uumbaji wa ulimwengu huu mkubwa ni ukamilifu na kukaribia zaidi kwa mwanadamu kwenye chanzo cha ukamilifu wote, yaani Mwenyezi Mungu Mtukufu, basi ili kufikia lengo hili kuu, ni lazima kuwe na nyenzo na njia zitakazomwezesha mwanadamu kukaribia kwa Mwenyezi Mungu. Ndiyo maana serikali ya kimataifa ya Imamu wa Zama—‘Ajjalallāhu Taʿālā Farajahu ash-Sharīf—inalenga kuweka nenzo zaa takarrub (kukurubiana na Mwenyezi Mungu) na kuondoa vizuizi vyote vilivyoko katika njia hii.
Bila shaka, mwanadamu ni mchanganyiko wa mwili na roho, na mahitaji yake pia yamegawanyika katika mambo ya kimada na ya kiroho. Kwa hiyo ili afikie ukamilifu wa kweli, ni lazima asonge mbele katika nyanja zote mbili kwa mpangilio na kwa makadirio sahihi. Aidha, "uadilifu" ambao ni tunda kubwa la utawala wa Kiungu, ndiyo dhamana ya ustawi na salama ya mchakato wa ukuaji wa mwanadamu katika safari ya kimwili na kiroho.
Kwa hivyo, malengo ya serikali ya Imamu wa Kumi na Mbili (as) yanaweza kuelezewa kwa mihimili miwili: "ukuaji wa kiroho" na "utekelezaji wa haki na uenezi wake".
Ukuaji wa Kiroho
Katika kipindi chote cha maisha ya mwanadamu mbali na utawala wa Hujja wa Mwenyezi Mungu, je, nafasi ya uadilifu na maadili ya kiroho imekuwaje? Je, si kweli kwamba binadamu siku zote amekuwa akitembea katika njia ya kuporomoka kiroho? Na kwa kufuata matamanio ya nafsi na vishawishi vya Shetani, amesahau uzuri wa maisha yake na kwa mikono yake ameuzika katika kaburi la matamanio?
Kwa muhtasari, tunaweza kusema kuwa: m'anawi katika maisha ya mwanadamu ndio yanayoivuta pumzi ya mwisho kabisa, na hata katika maeneo mengi ya dunia na kwa watu wengi, haijasalia athari yoyote ya m'anawi.
Serikali ya hazina ya mwisho ya Mwenyezi Mungu inafanya juhudi katika kuufufua upande huu wa kiroho wa mwanadamu, ili amwonjeshe ladha tamu ya maisha ya kweli, na kuwafanya watu wote wakumbuke kwamba tangu mwanzo walikuwa wamekadiriwa kuishi maisha hayo. Kama ambavyo Qur’ani Tukufu inasema:
"یَا أَیُّهَا الَّذِینَ آمَنُوا اسْتَجِیبُوا لِلَّهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاکُمْ لِمَا یُحْیِیکُمْ."
“Enyi mlioamini! Mwitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapokuiteni kwa kitu kitakachokupeni uhai. ”(Surat al-Anfāl, Aya ya 24)
Kwa hiyo, maisha ya kiroho ambayo ni alama ya pekee ya mwanaadamu dhidi ya wanyama, ni sehemu kuu na msingi wa uwepo wa mwanadamu. Ndio maana, wakati wa utawala wa Khalifa wa Mwenyezi Mungu, sehemu hii ya kiini cha mwanadamu hupangiliwa vizuri, na maadili ya kibinadamu hupata nafasi na nzuri katika kila nyanja ya maisha.
Uenezi wa Uadilifu
Jeraha kubwa zaidi katika mwili wa jamii ya wanadamu tangia zama za kale hadi sasa, limekuwa ni dhuluma na uonevu uliopo katika jamii ya wanadamu. Binadamu siku zote wamekuwa wakizuiwa kupata haki zao katika nyanja mbalimbali, na kamwe neema za kimwili na kiroho hazijagawanywa kwa haki miongoni mwa watu. Wakati wowote kulikuwepo matumbo yaliyojaa vyakula, palikuwepo pia kundi la watu waliokufa kwa njaa; karibu na majumba ya kifahari kulikuwepo watu waliolala mitaani na kwenye vijiwe. Mwanadamu daima alikuwa katika hamu ya kufikia haki na usawa, akiisubiri kwa shauku enzi ya ustawi wa uadilifu.
Mwisho wa kungojea huko ni zama za kijani za utawala wa Imamu Mahdi (‘Ajjalallāhu Farajahu). Yeye atakuwa kiongozi mkuu wa haki na imamu wa uadilifu, ambaye atatekeleza uadilifu katika dunia yote na katika nyanja zote za maisha. Ukweli huu mtamu umetajwa katika riwaya nyingi zinazobashiria kuja kwake. Imamu Husein—‘Alayhis-salaam—anasema:
"لَوْ لَمْ یَبْقَ مِنَ اَلدُّنْیَا إِلَّا یَوْمٌ وَاحِدٌ لَطَوَّلَ اللّٰهُ عَزَّ وَجَلَّ ذَلِکَ اَلْیَوْمَ حَتَّى یَخْرُجَ رَجُلٌ مِنْ وُلْدِی فَیَمْلَأَهَا عَدْلًا وَقِسْطًا کَمَا مُلِئَتْ جَوْرًا وَظُلْمًا، کَذَلِکَ سَمِعْتُ رَسُولَ اللّٰهِ صَلَّى اللّٰهُ عَلَیْهِ وَآلِهِ یَقُولُ."
“Kama isingebakia katika dunia isipokuwa siku moja tu, basi Mwenyezi Mungu angeifanya siku hiyo kuwa ndefu ili mtu kutoka katika kizazi changu atoke na kuijaza dunia kwa haki na uadilifu, kama ilivyojaa dhuluma na uonevu. Hili nimelisikia kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw). "(Kāmāl ad-Dīn, J. 1, uk. 317)
Na kuna riwaya nyingi nyingine zinazobashiria uadilifu wa kimataifa na kung’olewa kwa dhuluma na mizizi yake chini ya kivuli cha serikali ya mja wa mwisho wa ahadi ya Mwenyezi Mungu.
Utafiti huu unaendelea...
Imenukuliwa kutoka katika kitabu cha “Negin-e Āfarinish” (Lulu ya Uumbaji) huku ikifanyiwa marekebisho kiasi.
Maoni yako